Wednesday, September 16, 2020

BAADA YA KENYA KUKUBALI "YAISHE" TANZANIA NAYO YARUHUSU NDEGE ZA KENYA KUTUA NCHINI

IKIWA ni takriban saa 24 tangu Kenya itangaze kuiweka Tanzania kwenye orodha ya nchi ambazo raia wake hawatalazimika kukaa karantini ya siku 14 kwa sababu ya ugonjwa wa Corona endapo wataingia ndani ya mipaka ya Kenya, Tanzania nayo kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA leo Septemba 16, 2020 imetoa taarifa ya kuruhusu ndege za Kenya ikiwemo Kenya Airways kutua kwenye viwanja vya ndege vya Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na kusainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Bw. Hamza Johari leo Jumatano Septemba 16, 2020, imesema tayari Mamlaka ya Usafiri wa Anga Kenya imejulishwa juu ya uamuzi huo wa Tanzania na kwamba kuanzia leo Mashirika ya ndege ya Kenya Airways, Fly 540 Limited, Safarilink Aviation, AirKenya Express Limited yameruhusiwa kufanya shughuli zake nchini kuanzia leo.
Habari za awali za Kenya kuiongeza Tanzania kwenye orodha yake ya mataifa ambayo raia wake hawatakaa karantini ya siku 14 ni hii hapa.....NA K-VIS BLOG/MASHIRIKA YA HABARI

HATIMAYE serikali ya Kenya imeiorodhesha Tanzania kati ya nchi ambazo raia wake wanaruhusiwa kuingia nchini humo bila kulazimishwa kuwekwa karantini ya siku 14 kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona.

Uamuzi huo wa Serikali ya Kenya ulitangazwa Septemba 15, 2020 katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa idara ya uhamiaji nchini Kenya Alexender Muteshi ambapo Tanzania iko kwenye namba 132.

Awali Kenya ambayo ni Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, Burundi, Rwanda, Uganda na Sudani Kusini ilitoa orodha ya mataifa ambayo raia wake hawalazimiki kukaa karantini ya siku 14 waingiapo nchini humo lakini Tanzania na Burundi hazikuwekwa kwenye orodha hiyo, hali iliyozusha hasira kutoka Tanzania ambayo nayo kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) ikatoa taarifa ya kufuta kibali cha ndege za Kenya kutua nchini Tanzania. 
 

0 comments:

Post a Comment